WATAALAMU WAZAWA WAPEWE NAFASI KWENYE MIRADI MIKUBWA.
Na Angelina Mganga,DmNewsOnline
DAR ES SALAAM
MKUU wa Wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam Edward Mpogolo amesema serikali imeendelea kuwapatia mafunzo ya kuwajengea uwezo wataalamu wa sekta ya ujenzi wakiwemo wabunifu majengo,wakadiriaji majenzi na wakandarasi ili waweze kupata fursa kwenye miradi mikubwa.
Mpogolo amesema hayo Oktoba 29,2024 alipomwakilisha Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt .Doto Biteko kwenye ufunguzi wa mkutano mkuu wa Tano wa Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB) uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano ya Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam .
Aidha amewataka wataalamu na kampuni za ndani kuchangamkia fursa na kushiriki katika michakato ya zabuni za miradi mikubwa ili kujijengea uwezo wa kitaalamu na kupunguza utegemezi wa wataalumu kutoka nje kwa kazi za ujenzi na matengenezo.
Pia amesema kwamba Serikali imeendelea
kutoa hamasa kwa wataalamu wa ndani kuchangamkia fursa ya miradi inayoendelea kufanyika nchini.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB) Dkt.Ludigija Bulamile amesema bodi hiyo imesajili wahitimu waliomaliza masomo yao vyuo vikuu na kwamba lengo ni kuhakikisha wahitimu wote wanasajiliwa ndani ya kipindi cha miaka miwili baada ya kuhitimu masomo yao.
Amesema kuwa mwaka 2005 Bodi ilianzisha mpango wa mafunzo kwa vitendo ya kuwaimarisha wahitimu wa vyuo vikuu na kwamba kutokana na jitihada za Wizara ya Ujenzi kufadhiri mafunzo kwa wahitimu.
Dkt.Bulamile amesema kuwa bodi imekua ikifanya ukaguzi wa miradi mbalimbali ili kuhakikisha ubora wa majengo na usalama wa raia na mali zao.
Comments
Post a Comment