MBUNGE ULENGE NA JITIHADA ANAZOZICHUKUA KUMUUNGA MKONO SAMIA UBORESHAJI ELIMU TANGA



Na Yusuph Mussa,DmNewsOnline
 TANGA 
                      
MBUNGE  wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga Mhandisi Mwanaisha Ulenge anasema Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan tangu aingie madarakani Machi 19, 2021 amekuwa anafanya kazi kubwa katika kuboresha huduma za jamii ikiwemo elimu, afya na maji.

Mhandisi Ulenge anasema Dkt. Rais Samia amefanya yote hayo ikiwa ni Utekelezaji wa Ilani ya CCM 2020-2025.
Na ilani ya CCM katika kipengele cha elimu, malengo yake ni kuzalisha rasilimali watu bora kwa maendeleo  ya kijamii na kiuchumi.

"Hivyo, Serikali imetimiza wajibu wake, ni wajibu wetu  sisi wananchi kuunga mkono jitihada za Serikali ya CCM  kwa kuhakikisha tunaitumia vema miundombinu bora ya elimu ili  jamii yetu  izalishe rasilimali watu bora kwa maendeleo  ya jamii yetu na Taifa letu kwa jumla" anasema Mhandisi Ulenge. 

Ulenge ameongeza kuwa katika matokeo ya kidato cha nne bado kuna idadi kubwa ya ufaulu wa daraja la nne na sifuri.
Ni lazima wazazi na walimu washirikiane kuhakikisha wanaboresha ufaulu huo ili kuongeza idadi ya wanafunzi kuendelea na elimu ya juu hadi vyuo vikuu, huku utoro na kukosekana chakula cha mchana shuleni ikiwa ni miongoni mwa  changamoto zinazochangia ufaulu wa madaraja ya chini. 

"Elimu ni wajibu na elimu ni ibada, hivyo sio jambo la hiyari. Kusoma tumeamrishwa na Mungu wetu. Kwenye Quran takatifu tumeambiwa "Tusome kwa jina la Mola wetu aliyeumba kila kitu"  na hadithi inasema kuwa "Tumetakiwa tukaitafute elimu hata kwa kwenda nchi ya mbali". Biblia imesema, "Mshike rafiki elimu wala usimuache aende zake" hayo ni maneno ambayo Mhandisi Ulenge amekuwa akiwaeleza wanafunzi kila alikokwenda, huku akisisitiza, hakuna njia fupi ya kuyaendea mafanikio katika maisha, bali ni lazima tusome

Kwenye ziara yake aliyoifanya hivi karibuni kwenye halmashauri zote 11 za Mkoa wa Tanga pamoja na mambo mengine, Mhandisi Ulenge aliwahamasisha wanafunzi kupenda shule, na hasa wanafunzi wa kike ambao wameonekana wanakabiliana na changamoto nyingi kwenye safari yao ya kimaisha katika kutafuta elimu.

Moja ya changamoto hizo ni mimba za utotoni, mazingira magumu ya kujisomea wakiwa nyumbani, ukosefu wa mabweni ama hostel ili wanafunzi hao wa kike wasome huku wakiwa wanaishi shuleni. Umbali mrefu wa kwenda shule na kurudi nyumbani, tena wakiwa wanatembea kwa miguu, na vishawishi wanavyofanyiwa njiani ili wapewe lifti ya pikipiki maarufu kama bodaboda, na kurubuniwa kimapenzi.

Mhandisi Ulenge akiwa kama Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amekuwa anaunga mkono juhudi za Rais Dkt. Samia kwa kutoa fedha ili kukamilisha ujenzi wa nyumba za walimu, vyumba vya madarasa na ofisi za walimu.

Pia katika kukuza taaluma, ameweza kutoa kompyuta kwa Shule ya Sekondari Chifu Mang'enya iliyopo wilayani Muheza, Shule ya Sekondari Rashid Shangazi iliyopo Mlalo, Wilaya ya Lushoto, na Shule ya Sekondari Old Tanga, ambapo kila shule imepata kompyuta tano, printer na projector. Vifaa hivyo kila shule vikiwa na thamani ya sh. milioni 15.

Akiwa kwenye ziara hiyo hivi karibuni, Mhandisi Ulenge anasema alifika Shule ya Sekondari Mfundia iliyopo Kata ya Kerenge, Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe mwaka 2022 na kutoa sh. 600,000 kwa ajili ya kuweka milango miwili ya chuma bweni la wanafunzi, na kisha kufanya harambee, ambapo katika harambee hiyo, wanawake wa UWT walichangia sh. 200,000 zilizoweka madirisha mawili kwenye bweni hilo.

 Mhandisi Ulenge alikuta ujenzi wa bweni hilo ulianza tangu mwaka 2015, lakini umeishia kwenye kupaua na kuwekewa milango miwili na madirisha mawili. Na ili kukamilika kunahitajika sh. milioni 50, na katika mchango wake, akatoa tena mifuko 20 ya saruji ili kuweka sakafu.

"Rais Dkt  Samia Suluhu Hassan anafanya kazi kubwa katika kuhakikisha anaboresha huduma za jamii kwenye Taifa letu. Lakini anafanya jitihada kubwa za kuinua uchumi wa Taifa letu kwa mtu mmoja mmoja, na Taifa kwa ujumla. Hivyo, mimi kama Mbunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nawiwa kuchangia maendeleo hayo.

"Mwaka 2022 nilikuja hapa nikachangia ujenzi wa bweni na nikatoa fedha (sh. 600,000) kwa ajili ya milango miwili kwenye bweni hilo. Lakini pia nikafanya harambee, na wanawake wa UWT wakachangia fedha (sh. 200,000). Na kwenye mkutano huu, wanafunzi wamenieleza na kuweza kunitoa machozi, kuwa bado bweni hilo halijakamilika, na hata mimi nimelikagua, ni kweli halijakamilika. Sasa natoa saruji mifuko 20 ili liwekwe sakafu"  anasema Mhandisi Ulenge.

Mhandisi Ulenge ambaye pia ni Mbunge wa Bunge la Dunia (IPU), aliwaeleza wazazi, walimu na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mfundia kuwa yupo tayari kuwa mlezi wa shule hiyo, lakini kwa sharti moja, wanafunzi waweze kufanya vizuri kwenye masomo yao. Kwani, matokeo aliyooneshwa ya kuanzia mwaka 2022 na 2023 sio mazuri, hivyo akataka ushirikiano wa wazazi, walimu na wanafunzi kuweka nguvu za pamoja kuona wanafuta sifuri na daraja la nne (division four).

"Nipo tayari kuwa mlezi wenu lakini kwa sharti wanafunzi waweze kufanya vizuri sababu matokeo ni mabaya. Ili kufikia hatua hiyo ni lazima kuwe na ushirikiano kati ya wazazi, walimu na wanafunzi. Na nataka kwa kuanzia tufute division zero, na division four. Nia yangu ni kuona wahandisi, madaktari na watu wenye taaluma mbalimbali wanatoka  Mkoa wa Tanga.

"Serikali imefanya wajibu wake kwa kujenga miundombinu bora ya elimu. Nini wajibu wa sisi wananchi, na nini wajibu wa mtoto wa Tanga! na Nini wajibu wa Mwalimu wa Tanga kuona taaluma ya watoto wetu inakuwa na kuleta mafanikio kwa mtu mmoja mmoja na Taifa!" alihoji Mhandisi Ulenge.

Akiwa Shule ya Sekondari Mgombezi iliyopo Halmashauri ya Mji Korogwe, Mhandisi Ulenge anasema Rais Dkt. Samia  amepeleka fedha nyingi za kujenga miundombinu ya shule, hivyo anatamani miundombinu hiyo iende sambamba na ufaulu kwa wanafunzi kwa kufanya  vizuri kwenye masomo yao.

"Dkt. Samia Suluhu Hassan amejenga miundombinu bora ya elimu, na Mkuu wa Shule amezungumza kwenye taarifa yake fedha zilizoletwa Mgombezi kwa ajili ya elimu. Katika mipango iliyokuwepo ya kuhakikisha shule inakuwa na kidato cha tano na sita, mimi natamani miundombinu bora iliyoletwa na Dkt. Samia iweze kuleta tija iliyo bora zaidi katika elimu mkoa wetu wa Tanga.

"Majengo yaliyoletwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan yanaweza kuwa sawa na mapambo tu iwapo hatutawekeza juhudi za makusudi kuhakikisha tunaongeza ufaulu katika shule zetu. Kwa hiiyo watoto wangu wapendwa nimekuja kwenu leo ili kuwatia moyo  katika suala zima la elimu. Niliyesimama mbele yenu kitaaluma ni Mhandisi, na ili iweze kuwa Mhandisi ni lazima uwe umefaulu vizuri masomo ya kemia, fizikia na hisabati" anasema Mhandisi Ulenge.

Mhandisi Ulenge akizungumza na wazazi, walimu na wanafunzi Shule ya Msingi Lwandai iliyopo Kata ya Mlalo, Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto ambayo pia wanasoma wanafunzi wenye mahitaji maalumu, aliwataka wazazi kuwapeleka shule watoto wenye ulemavu, sababu kuwa na mtoto mwenye ulemavu sio laana bali ni baraka.

Mhandisi Ulenge ambaye alifika kwenye shule hiyo ili kuwaona wanafunzi wenye mahitaji maalumu, anasema Serikali ya Dkt. Samia imewajengea darasa la kipekee lenye kila kitu kwa sababu na wao wanahitaji kupata elimu wakiwa kwenye mazingira bora.

"Wazazi wasiwafiche watoto wenye ulemavu wa aina yeyote ile, bali wanatakiwa kuwatoa na kuwapeleka shule ili wapate elimu kama ilivyo kwa watoto wengine. Nataka kuwaambia ndugu zangu, mtoto kuwa mlemavu sio laana bali ni baraka, hivyo mnatakiwa kuwapeleka shule nao wapate elimu.

"Watoto wenye usonji, nyuma yake kuna baraka kubwa, hivyo tuwaenzi na kuwaona ni watu ambao wakipata elimu wataweza kumudu maisha yao, na kuweza kuwasaidia wengine. Nimesikia kuna mahitaji yanatakiwa, lakini mimi nataka kuanza kwa kutoa Bima ya Afya kwa hawa watoto 30 waliopo kwenye hili darasa, watakaa kama familia sita sita ili kutengeneza familia tano ambazo zitapatiwa matibabu" anasema Mhandisi Ulenge.

Mhandisi Ulenge anssema moja ya mahitaji ya watoto hao ni kujengewa bweni ili waweze kuishi hapo hapo shuleni, lakini pia kupatiwa walimu, kwani hadi sasa hawana mwalimu hata mmoja mwenye taaluma ya elimu maalumu.

Awali, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Lwandai Nasibu Muya, anasema shule yake ina jumla ya vitengo vitatu, Elimu Msingi darasa la awali hadi la saba, Kituo cha Elimu Ufundi, na Kituo cha Elimu Maalumu, ambapo Kituo cha Elimu Maalumu kina wanafunzi 30, wavulana wakiwa 18 na wasichana 12 ambao wana aina tofauti za ulemavu ikiwemo usonji, viungo na akili.

"Katika mafanikio, wapo wanafunzi watano waliokamilisha hatua  zote tatu za ujifunzaji katika kitengo na stadi mbalimbali, na kuweza kuandikishwa elimu msingi, ambapo hadi sasa wapo wanafunzi wanne wanasoma darasa la nne, wavulana watatu na msichana mmoja wa darasa la tatu. Na Serikali imewajengea darasa moja na matundu matatu ya vyoo kupitia Mradi wa BOOST 2022/2023, na wanapata chakula cha mchana shuleni kwa ruzuku ya Serikali.

"Kitengo hiki kina changamoto ikiwemo ukosefu wa walimu wenye taaluma ya uhitaji maalumu, na baadhi ya wanafunzi kutofika shuleni kwa wakati kutokana na umbali na changamoto za ulemavu wao. Lakini mapendekezo yetu, kituo kijengewe mabweni kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavu uliozidi ili wapatiwe  huduma muda wote" alisema Muya.

Akiwa Shule ya Sekondari Rashid Shangazi iliyopo Kata ya Mlalo, Mhandisi Ulenge aliwataka wanafunzi kusoma kwa bidii ili kurudisha fadhila kwa Serikali, kwani imejenga miundombinu ya madarasa na nyumba za walimu kwa fedha nyingi, hivyo ni lazima waoneshe uzalendo kwa kusoma kwa bidii, huku wakiziishi ndoto zao, huku wakitakiwa kujifunza kwa waliofanikiwa.

Mhandisi Ulenge akiwa Shule ya Sekondari ya Wasichana Sindeni ya kidato cha tano na sita iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, aliitaka Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Handeni (HTM) kupeleka maji ya uhakika kwenye shule hiyo. Kwani pamoja na jitihada alizozikuta hapo za kuchimba maji ya visima vifupi, bado haitoshi, kwani wanafunzi hao ni wengi, na hasa ukichukulia hao ni watoto wa kike.

Kwenye shule hiyo ambayo inafanya vizuri kwenye masomo ya sanaa, alitoa zawadi kwa wanafunzi 10 wa kidato cha sita waliofanya vizuri kwenye mitihani ya majaribio kwa masomo ya HGK na HGL kwa wale waliopata Daraja la Kwanza la pointi tatu hadi tano

Akiwa Shule ya Sekondari Misima ya kidato cha kwanza hadi sita, aliwataka walimu kuwasaidia wanafunzi kufanya vizuri kwenye masomo yao. Ni baada ya shule hiyo kuonekana ina matokeo ya chini, na kutoa motisha ya sh. 10,000 kila mmoja kwa wanafunzi 10 wa kidato cha kwanza waliofanya vizuri kwenye mitihani ya majaribio.

Lakini pia, katika shule za msingi na sekondari zaidi ya 10 alizotembelea Mkoa wa Tanga, alitoa sh. milioni saba kwa ajili ya kununua mchele na mahitaji mengine, hasa kwa wanafunzi waliokuwa wanajiandaa na mitihani ya kitaifa.

ATOA ZAWADI YA TAULO ZA KIKE NA FEDHA

Ili kutoa hamasa kwa watoto wa kike kupenda kusoma na kufaulu masomo, Mhandisi Ulenge ametoa zawadi ya taulo za kike kwa wanafunzi waliofanya vizuri kwenye mitihani ya ndani ya shule, ile ya ngazi ya wilaya na mkoa, na ile ya kitaifa, na kuambatana na fedha.

Lakini hata waliojibu maswali vizuri mara baada ya kuulizwa mambo mbalimbali ya kitaaluma na kijamii, pia aliwapa fedha wavulana kwa wasichana kwenye shule zote alizotembelea, ambapo jumla ya taulo za kike alizotoa kwa shule zote alizotembelea ni boksi 35 zikiwa na thamani ya sh. 2,940,000. Na wanafunzi waliojibu maswali yake walipewa sh. 270,000.

MAKTABA ZA MKOA WA TANGA

Kwenye ziara ya Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango aliyoifanya mkoani Tanga, Mhandisi Ulenge alimueleza, Maktaba ya Tanga Jiji ni chakavu na ni kongwe kuliko Uhuru wa nchi yetu. Na hali yake ndani ni chakavu mno, huku ikiwa haina vitabu, ambapo Dkt. Mpango akaelekeza Maktaba ikarabatiwe na vitabu viletwe, na  kweli baada ya muda vitabu vililetwa na mpango wa ukarabati ukaanza

Akichangia bungeni, Mhandisi Ulenge anasema  kuwa, maktaba za wilaya ziboreshwe, kwani maktaba sio majengo ya makumbusho, bali zinapaswa ziwe za kisasa, na walimu na wazazi wawahimize watoto waweze kuzitumia kwa ajili ya kuongeza uelewa, elimu, na weledi wa mambo mengine ya kitaaluma na kijamii.



Comments

Popular posts from this blog

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE TAMISEMI YAKOSHWA NA UBORA WA MIRADI YA MAENDELEO KIBAHA TC

MAMBO 10 MAZITO YANAYOIANGAMIZA NA KUIZAMISHA CHADEMA 2024/2025