WANASIASA NCHINI WATAKIWA KUFANYA SIASA ZA KUTUMIA LUGHA ZA STAHA
Na mwandishi wetu,DmNewsOnline
DAR ES SALAAM
KATIBU Mkuu wa Chama cha National League for Democracy (NLD), Doyo Hassan Doyo amewataka wanasiasa nchini kufanya siasa za kistaarabu na kutumia lugha za staha na sio siasa za kudhalilisha na kuchafua watu kwa kutweza utu wao.
Kauli hiyo imetolewa Septemba 29,2024 na Katibu Mkuu wa NLD Doyo Hassan katika Uzinduzi wa program ya operesheni ya fyeka CCM kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa 2024 uliofanyika katika ofisi za Makao makuu ya chama hicho zilizopo Tandika Wilaya ya Temeke Jijini Dar es Salaam.
"Juzi Kuna Kongamano la chama fulani la wanawake lilikuwa likimtuhumu Rais kuwa ni muuaji hiyo siyo sawa kwani kama Mungu amekupangia kifo utakufa tuu"amesema Doyo
Amesema kuwa chama hicho kimesikitishwa na tuhuma za chama hicho na kuviomba vyombo vya usalama kuchukua hatua stahiki kwa wanaomchafua Rais
"Chama kitafanya siasa safi na kutoa wito kwa wanachama wake kutotoa maneno ya kashfa na kutweza utu wa mtu na waheshimu Mamlaka kwa kuwa na Uhuru wenye mipaka",amesema
Hata hivyo ameongeza kuwa katika itikadi ya chama chetu tunaamini kuwepo kwa Uhuru wenye mipaka na wa kujenga hoja juu ya namna gani wanaweza kuwasaidia watanzania kutatua changamoto zao na si kutuka diwani,mbunge au Rais wa nchi hivyo nawasihi wanachama wa NLD mkawaambie watanzania namna mtakavyowakwamua na kujenga hoja za kuleta maendeleo.
Pia amelalamikia ratiba ya uchaguzi wa serikali za mitaa ambayo imebana na haitoi muda wa kutosha lwa vyama kujiandaa na kujipanga vyema.
" Tunaiomba TAMISEMI isipime vyama vyetu kwamba vinaweza kushindana na chama tawala kwa kufanya kampeni kwa muda wa siku Saba pekee,hivyo tunaomba ratiba iongezwe muda ili tuweze kumudu hali ya uchaguzi kwani kwa namna vyama vyetu hali zake zilivyo inaleta shida na hatusemi uchaguzi uhairishwe huo siyo msimamo wetu tunaomba tu ziongezwe siku ili tujipange vizuri",amesema.
Doyo amesema chama hicho kitasimamisha wagombea katika uchaguzi wa serikali za mitaa na tayari timu yake iko Mikoani kuhakikisha wagombea wanapatikana.
Kwa upamde wake Katibu Mkuu mstaafu wa NLD Tozi Matwanga amesema kuwa ili kujenga serikali ni lazima chama kiingie katika uchaguzi,hivyo na wao kama chama watashiriki chaguzi zote .
Hata hivyo chama hicho kimewapokea wanachama wapya kutoka chama cha ACT Wazalendo na ADC akiwemo Mariam Ahmed Sijaona ambaye alikuwa mjumbe wa halmashauri kuu ngome ya wanawake Taifa ya ACT Wazalendo ambaye amesema amechukua maamuzi ya kukihama na kujiunga na NLD baada ya kusoma na kuridhishwa na Sera za Chama
Comments
Post a Comment