RC CHACHA APONGEZA KASI YA UKUSANYAJI MAPATO KALIUA
Na Allan Vicent,DmNewsOnline
TABORA
OFISI ya Mkurugenzi, Madiwani, Wataalamu na Watendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Kaliua Mkoani Tabora wamepongezwa kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo na kasi nzuri ya ukusanyaji mapato kutoka katika vyanzo vyake.
Pongezi hizo zimetolewa na Mkuu wa Mkoa huo Paul Matiko Chacha alipokuwa akizungumza na watendaji hao katika kikao maalumu cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo cha mapitio ya taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG).
Amesema kuwa halmashauri zote 8 za Mkoa huo zinafanya vizuri lakini halmashauri Kaliua ina kasi kubwa zaidi kwani mwishoni mwa mwezi Mei 2024 walikuwa wamekusanya sh bil 6.5 ambazo ni zaidi ya asilimia 100 ya malengo yao.
RC Chacha amebainisha kuwa kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Mkoa huo ulikisia kukusanya jumla ya sh bil 39 kutoka katika vyanzo vyake vya ndani lakini kabla ya mwaka wa fedha kumalizika kiasi cha sh bil 33.4 zilikuwa zimekusanywa.
‘Nawapongeza kwa mshikamano mzuri wa kiutendaji, ila wale wote wanaozembea kwa namna moja au nyingine na kukwamisha utekelezaji miradi ya maendeleo msiwafumbie macho, wachukulieni hatua mara moja’, amesema.
Aidha Mkuu wa Mkoa ameagiza kila Mkuu wa Kitengo na Divisheni katika halmashauri hiyo kutimiza wajibu wake ipasavyo na kuelekeza Ofisi ya Mkurugenzi kuchukua hatua stahiki kwa wale wanaoenda kinyume.
Kuelekea kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu , amewataka madiwani kuitisha mikutano ya hadhara na kuwaeleza wananchi mazuri yote yaliyofanywa na serikali yao inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.
Pia amewataka kutoa taarifa ya miradi yote inayosuasua katika kata zao kwa Mkurugenzi ili taratibu zifanyike na utekelezaji miradi hiyo uendelee.
Kuhusiana na taarifa ya CAG, RC amemwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Jerry Mwaga kuhakikisha hoja zote zilizoibuliwa na Mkaguzi zinafanyiwa kazi haraka ili kabla ya mwezi Julai ziwe zimepatiwa majibu na kufungwa.
Akihitimisha kikao hicho Mwenyekiti wa Halmashauri Japhael Lufungija amemhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa wamepokea maelekezo yote aliyoyatoa na watayafanyia kazi kwa wakati.
Amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwaletea fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji miradi ya maendeleo na kubainisha kuwa fedha zote zimetumika kwa kazi iliyokusudiwa na kusimamiwa ipasavyo.
Aidha amemhakikishia RC Chacha kuwa wataendelea kulinda maadili ya jamii kwa kufichua, kukamata na kuwachukulia hatua wale wote wanaojihusisha na vitendo vya ushoga, ubakaji ikiwemo kuua watu wenye albinism.
Comments
Post a Comment