KANISA LATOA MSAADA WA CHAKULA KWA KAYA ZAIDI YA 100




Na Allan Vicent,DmNewsOnline
TABORA

KANISA la Tanzania Assemblies of God (TAG) Maranatha Miracle Centre lililopo eneo la Cheyo katika Halmashauri ya Manispaa Tabora limetoa msaada wa chakula kwa kaya zaidi ya 100 zenye uhitaji mkubwa ili kuwawezesha kuishi.

Akizungumza na DmNewsOnline Leo Juni 26 ,2024  Mchungaji Kiongozi wa Kanisa hilo Rev.Lutengano Mwasongela amesema kuwa wametoa msaada huo kama sehemu ya mchango wa kanisa hilo kwa jamii inayowazunguka ili kudumisha mahusiano mazuri.

Ameongeza kuwa wametoa mchango huo ili kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya 6 inayaoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha jamii ya Watanzania haifi na njaa.

Rev.Mwasongela amebainisha kuwa kanisa lake limekuwa likitoa msaada huo kwa nyakati tofauti ikiwemo kipindi cha sikukuu za pasaka na krismas kwa lengo la kurejesha furaha katika mioyo ya waliokata tamaa.

Amefafanua kuwa katika wiki kanisa la TAG Maranatha Miracle Centre limeendeleza utaratibu huo kwa kufanya matendo mema kwa jamii ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 19 tangu kuanzishwa kwake mjini hapa.

Aidha ameongeza kuwa maadhimisho hayo yanaenda sambamba na maadhimisho ya miaka 85 tangu kuanzishwa kwa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) hapa nchini ambapo kilele cha maadhimisho hayo Kitaifa itakuwa Julai 14, 2024.

‘Tuna kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa kanisa letu la TAG Maranatha Miracle Centre kufikisha umri huo na Kanisa Mama la TAG kufikisha miaka 85 tangu lianzishwe hapa nchini, tunajivunia mafanikio makubwa sana’, amesema.

Rev.Lutengano amebainisha kuwa katika wiki ya maadhimisho hayo mbali na kutoa msaada wa chakula pia wametoa msaada wa vifaa vya elimu na taulo za kike kwa watoto wa shule za msingi na sekondari zilizoko katika kata ya Cheyo.

Aidha kanisa hilo pia limefanya mkutano wa injili na kutoa msaada wa chakula kwa kaya 5 zenye uhitaji zilizoko katika kata ya Ipuli na katika kuokoa maisha ya wananchi walioko hospitalini waumini walijitolea zaidi ya lita 20 za damu.

Akiainisha mafanikio waliyopata katika kipindi cha miaka 19, Rev.Lutengano amesema kuwa kanisa hilo limeanzisha matawi 9 Mkoani hapa na 5 nchini Burundi na limesomesha wachungaji 7 na watoto 8 wa kaya maskini wamepelekwa shule.

Waumini wa kanisa hilo nao wameongezeka hadi kufikia 657 ambapo watu wazima wanaume ni 181, wanawake 324, watoto wa kiume 64 na wa kike 88 na wameanza ujenzi wa kanisa kubwa linalokadiriwa kugharimu sh mil 120.



Comments

Popular posts from this blog

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE TAMISEMI YAKOSHWA NA UBORA WA MIRADI YA MAENDELEO KIBAHA TC

MAMBO 10 MAZITO YANAYOIANGAMIZA NA KUIZAMISHA CHADEMA 2024/2025