JOTO LA UCHAGUZI WA MWENYEKITI CCM TABORA LAPANDA




Na Allan Vicent,DmNewsOnline
TABORA

WANACHAMA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoani Tabora wanasubiri kwa hamu kubwa kupata Mwenyekiti mpya wa Chama hicho atakayewaongoza kwenye kinyanga’anyiro cha Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu na Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani mwakani.  

Akizungumza na DmNewsOnline Leo Juni 26,2024  Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Mkoa, Idd Moshi amesema kuwa mchakato wa kujaza nafasi hiyo iliyoachwa wazi na aliyekuwa Mwenyekiti wao Mzee Hassan Mohamed Wakasuvi aliyefariki ghafla Februari 21 mwaka huu upo katika hatua za mwisho.

Amesema kuwa kwa sasa wanachosubiri ni uteuzi wa mwisho wa majina ya wagombea watakaoingia kwenye kinyang’anyiro cha kuomba ridhaa ya wanaCCM wa Tabora kupitia kura zao.

‘Muda wowote Kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kitaketi na kufanya uteuzi wa mwisho wa wagombea wa nafasi hiyo, baada ya zoezi hilo kukamilika na kuletewa majina tutawatangazia wana Tabora tarehe ya uchaguzi’, amesem

Komredi Idd amebainisha kuwa Uchaguzi ndani ya CCM ni wa kidemokrasia, kila mgombea ana haki sawa na mwenzake, hivyo akawataka wanaCCM na wagombea wote kukaa mguu sawa kwa utulivu wakisubiri tangazo la tarehe ya uchaguzi.

Aidha amewataka wagombea wote kutofanya kampeni ya aina yoyote ile katika kipindi hiki hadi watakapoletewa majina na kutangazwa utaratibu wa uchaguzi huo mdogo ambao unasubiriwa kwa hamu kubwa na wanaCCM na jamii kwa ujumla.

Ameonya kuwa chama hakitasita kumchukulia hatua mgombea yeyote atakayebainika kuanza kufanya kampeni kinyume na utaratibu na jina lake linaweza kuondolewa katika orodha ya wagombea.  

Komredi Idd amefafanua kuwa zoezi la uchukuaji fomu lilianza Aprili 6, 2024 na kumalizika Aprili 8, 2024 saa 10.00 jioni ambapo jumla ya makada 51 walijitokeza kuchukua fomu na kati yao 4 hawakurejesha fomu zao.

Amebainisha kuwa kati ya makada 51 waliochukua fomu, 45 ni wanaume na 6 ni wanawake na miongoni mwao ni Viongozi wa Chama katika ngazi mbalimbali, viongozi wa serikali na wanachama wa kawaida.

WanaCCM Janet Kaluli na Modesta Kayobe kutoka Wilaya ya Kaliua Mkoani hapa wamekiri kuwa hiki ni kipindi muhimu sana cha kupata Mwenyekiti mpya atakayeongoza chama kupata ushindi wa kishindo katika chaguzi zijazo.

Comments

Popular posts from this blog

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE TAMISEMI YAKOSHWA NA UBORA WA MIRADI YA MAENDELEO KIBAHA TC

MAMBO 10 MAZITO YANAYOIANGAMIZA NA KUIZAMISHA CHADEMA 2024/2025