DC ATAKA KUANZISHWA MIRADI YA KIELELEZO KALIUA
Na Allan Vicent,DmNewsOnline
TABORA
HALMASHAURI ya Wilaya ya Kaliua Mkoani Tabora imepongezwa kwa kuweka rekodi ya kufanya vizuri katika utekelezaji shughuli za maendeleo ya wanachi ikiwemo kuendelea kupata hati safi kila mwaka kwa kuweka vizuri taarifa zake.
Hayo yamebainishwa Leo Juni 26 ,2024 na Mkuu wa Wilaya hiyo Dkt.Rashid Chuachua alipokuwa akizungumza na Madiwani, Wataalamu na Watendaji wote wa halmashauri hiyo katika kikao cha kawaida cha baraza la madiwani.
Amesema kuwa halmashauri hiyo ni miongoni mwa halmashauri chache nchini zinazofanya vizuri sana katika suala zima la utekelezaji shughuli za maendeleo kupitia fedha zake za ndani na zile za serikali kuu ikiwemo kuingiza mapato mengi
Amesisitiza kuwa hayo yote yanachochewa kwa kiasi kikubwa na kazi nzuri yenye weledi na mshikamano mzuri wa Waheshimiwa madiwani, Wataalamu, Watendaji wa Vijiji na Kata na Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo Jerry Mwaga.
‘Halmashauri Kaliua inafanya kazi nzuri sana, na kila mwaka inavuka lengo la ukusanyaji mapato, naamini mnaweza kufanya zaidi ya hapo, ongezeeni ubunifu wa vyanzo vya mapato, ili kufanya makubwa zaidi’, amesema.
Dkt Chuachua ameshauri kuanzishwa kwa miradi ya kielelezo ambayo itaakisi mapato makubwa ya halmashauri na kuchochea maendeleo ya wananchi kwa kiasi kikubwa zaidi.
‘Najua halmashauri inafanya kazi kubwa, lakini kwa kuwa tunapata mapato mengi nashauri ianzishwe miradi ya kimkakati ya kielelezo ambayo mbali na kutoa huduma kwa wananchi pia itakuwa kichocheo kikubwa cha mapato’, amesema.
Ametoa mfano wa miradi hiyo kuwa ni kuanzishwa shule za mchepuo wa kiingereza, chuo cha kutoa huduma za afya, ufundi, miradi ya uzalishaji mali na mingine mingi, ili kuifanya halmashauri hiyo kuwa mfano wa kuigwa nchini.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Japhael Lufungija ameafiki ushauri huo na kumhakikishia Mkuu wa Wilaya kuwa wataufanyia kazi, alidokeza kuwa tayari wapo kwenye mchakato wa kuanzisha baadhi ya miradi ya kimkakati.
Ameongeza kuwa katika mwaka ujao wa fedha 2024/2025 halmashauri imetenga bajeti kwa ajili ya utekelezaji baadhi ya miradi ya kimkakati ili kuharakisha maendeleo ya wananchi na kuongeza mapato zaidi.
Comments
Post a Comment