MKOA WA PWANI YATUMIA TRILIONI 8.5 KUTEKELEZA MIRADI ITAKAYOPITIWA NA MWENGE.
Na Victor Masangu,DmNewsOnline KIBAHA
MBIO za Mwenge wa Uhuru umewasili leo rasmi mkoani Pwani ukitokea Mkoani Morogoro ambapo umekabidhiwa kwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani Alhaj Abubakar Kunenge ambapo utatembelea na kuzindua miradi mbali mbali ya maendeleo mkoani humo.
Akipokea Mwenge huo kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Adam Malima amesema kwamba katika mbio hizo mwenge huo utatembelea jumla ya miradi 126.
Kunenge amebainisha kwamba mbio za Mwenge huo wa uhuru kwa mwaka huu utakimbizwa katika Halmashauri tisa zilizopo katika Wilaya saba ambapo jumla ya kilometa 1,225.3 zitakimbizwa katika maeneo mbali mbali.
Kunenge amefafanua kwamba kati ya miradi hiyo miradi 18 itawekewa mawe ya msingi,miradi 22 itazinduliwa na miradi ipatayo 86 itakaguliwa.
Aidha Kunenge amesema kuwa miradi hiyo itagharimu kiasi cha shilingi Trilioni 8.536 ambapo serikali kuu imechangia bilioni 13.6,Halmashauri za wilaya shilingi bilioni 2.3 nguvu za wananchi na wawekezaji trilioni 8.5 na wadau wa maendeleo bilioni 14.6.
Pia amemshukuru Rais wa awamu ya sita kwa kuweka mazingira bora kwa ustawi na ufanisi zaidi katika sekta binafsi nchini.
Pia Kunenge katika hatua nyingine alisema kwamba katika kupambana na janga la ukimwi wameendelea kupambana kwa kutoa elimu ya upimaji wa wenza.
Kadhalika ameongeza katika kupambana na dawa za kulevya wameendelea kuimarisha mapambano kwa kubadilisha fikra,hisia na tabia.
Awali kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa Godfrey Mnzava alizitaka halmashauri zote za Mkoa wa Pwani kuhakikisha wanaandaa nyaraka zote za miradi ya maendeleo.
Comments
Post a Comment