LATRA WAPONGEZWA KUBORESHA HUDUMA ZA USAFIRI TABORA



Na Allan Vicent,DmNewsOnline 
TABORA

WAKAZI Mkoani Tabora wameipongeza Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kwa kuboresha huduma za usafiri barabarani na kupunguza kero na manyanyaso waliyokuwa wanapata abiria kwa kiasi kikubwa.

Pongezi hizo zimetolewa jana na baadhi ya wasafiri na wasafirishaji Mkoani hapa walipokuwa wakiongea na mwaandishi wa gazeti hili kuhusu mafanikio ya miaka 3 ya Rais wa awamu ya 6 Dkt Samia Suluhu Hassan.

John Johasy mkazi wa Isevya katika Halmashauri ya Manispaa Tabora alisema kuwa katika miaka 3 ya utawala wa Rais Samia huduma za usafiri barabarani zimeboreshwa kwa kiasi kikubwa sana tofauti na hali ilivyokuwa huko nyuma.

‘Tunawashukuru sana LATRA, wametusaidia kudhibiti ulanguzi wa nauli uliokuwa unafanywa na baadhi ya wasafirishaji, mawakala na wapiga debe wenye tamaa ya kujipatia faida kwa kuumiza wananchi’, amesema.     

Mmiliki wa vyombo vya usafiri Mkoani hapa, Said Juma Said maarufu kwa jina Yamelee alimpongeza Mkurugezi Mkuu wa LATRA, Meneja wa LATRA Mkoa na Maafisa wote wa Mamlaka hiyo kwa kufanya kazi kwa weledi mkubwa .

Amebainisha kuwa sasa hivi ukitaka leseni au kibali cha usafirishaji abiria husumbuliwi tena kama ilivyokuwa huko nyuma, hakuna rushwa, ukiomba leo unapata siku hiyo hiyo au kesho yake.

Zakayo Hussein mfanyabiashara, mkazi wa Wilaya ya Uyui Mkoani hapa alipongeza serikali ya awamu ya 6 kwa kuendelea kujenga barabara za lami na kuboresha kwa kiasi kikubwa usimamizi wa huduma za usafiri ardhini.

‘Changamoto za usafirishaji bidhaa, mizigo na hata abiria zimepungua sana kutokana na kazi nzuri inayofanywa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), tunaomba usimamizi huu uendelee hivi hivi’, amebainisha.

Kwa upande wake Afisa Mfawidhi wa Mamlaka hiyo Mkoani hapa Nelson Mmari alipongeza kazi nzuri iliyofanywa na inayoendelea kufanywa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha huduma za usafiri na usafirishaji zinaboreshwa.

Amebainisha katika kipindi cha miaka 3 ya Rais Samia, Mamlaka hiyo chini ya Mwenyekiti wake wa Bodi Profesa Ahmed Amen na Mkurugenzi Mkuu CPA Habib Suluo wamefanya kazi nzuri ambayo imepelekea kuboreshwa huduma za usafiri na usafirishaji nchini na kuahidi kuwa wataendelea kufanya makubwa zaidi.




Comments

Popular posts from this blog

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE TAMISEMI YAKOSHWA NA UBORA WA MIRADI YA MAENDELEO KIBAHA TC

MAMBO 10 MAZITO YANAYOIANGAMIZA NA KUIZAMISHA CHADEMA 2024/2025