RAIS SAMIA APELEKA BIL 5 KUCHIMBA BWAWA KUBWA LA MAJI URAMBO
Na Allan Vicent, DmNewsOnline
TABORA
WAKAZI wa Vijiji vya Kalemela A na B katika kata ya Muungano Wilayani Urambo Mkoani Tabora wamemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwapelekea kiasi cha sh bil 5.9 kwa ajili ya kutekelezwa mradi mkubwa wa Bwawa la Maji utakaowezesha wananchi kupata maji safi na salama ya kunywa.
Wakizungumza na gazeti hili juzi wamesema kuwa ujio wa mradi huo ni mkombozi kwao kwa kuwa utamaliza kilio chao cha miaka mingi cha ukosefu wa huduma ya maji safi na salama katika vijiji vyote vya kata hiyo na maeneo mengine.
Zebedayo Lukungu (50) mkulima, mkazi wa Kijiji cha Kalemela A ameeleza kuwa ukosefu wa maji safi na salama kwa wakazi wa vijiji hivyo ulipelekea wengi wao kuugua magonjwa ya kuhara mara kwa mara na ndoa nyingi kuvunjika.
‘Tunamshukuru sana mama yetu Rais Samia kwa kutuletea mradi huu, sasa tuna uhakika wa kunywa maji safi na salama ya bomba mwaka huu, tunachoomba mafundi waongeze bidii ili ukamilike kwa wakati’, amesema.
Mfanyabiashara Hussein Saidi (60) mkazi wa madukani katika Kijiji cha Kalemela B, amesema kuwa ujio wa mradi huo katika kata yao umesaidia vijana wengi kupata ajira za muda mfupi na wauza vifaa vya ujenzi kujipatia kipato.
Mwalimu Zena Sued wa shule ya msingi Kalemela ameishukuru serikali ya awamu ya 6 kwa kujali maisha ya wananchi wake na kutenga fedha kwa ajili ya kufikisha huduma ya maji safi na salama katika vijiji mbalimbali wilayani humo.
Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilayani humo Mhandisi Mapengu Gendai amefafanua kuwa mradi huo utakapokamilika utawezesha jumla ya vijiji 17 vyenye wakazi zaidi ya 148,000 kunufaika.
Ameongeza kuwa ujenzi wa mradi huo unaotekelezwa na Mkandarasi Kampuni ya Halem Construction ya Jijini Dar es salaam kwa gharama ya sh bil 5.9 ulianza mwezi Aprili mwaka jana na unatarajiwa kukamilika mwezi Novemba mwaka huu.
Amebainisha kuwa mradi huo utahusisha ujenzi wa tuta kubwa, utoro wa maji, magati ya kuchotea maji na eneo la kunyweshea mifugo na litakuwa na uwezo wa kukusanya maji kiasi cha mita za ujazo milioni 4.6.
Mhandisi Gendai ameongeza kuwa kati ya mita hizo za ujazo kiasi cha mita 3,331,637.17 zitatumika kwa matumizi ya binadamu na kiasi kilichobaki kitatumika kwa matumizi mengineyo ikiwemo kunyweshea mifugo.
Comments
Post a Comment