MANISPAA TABORA WAKABILIWA NA UPUNGUFU WA MADAWATI 9,500
Na Allan Vicent, DmNewsOnline
TABORA
HALMASHAULI ya Manispaa Tabora inakabiliwa na upungufu wa madawati 9,500 katika shule za msingi na sekondari ili kuwezesha kila mtoto kukaa kwenye dawati pindi wawapo darasani.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Wilaya ya Tabora Luis Bura alipokuwa akitoa taarifa ya hali ya miundombinu ya shule za msingi na sekondari katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC) kilichofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa halmashauri hiyo.
Amesema kuwa upungufu huo unapaswa kutatuliwa haraka iwezekanavyo ili kwenda na kasi ya maboresho makubwa ya miundombinu ya shule zote yanayoendelea kufanywa na serikali ya awamu ya 6 ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.
DC Bura amesisitiza kuwa ili kufanikisha upatikanaji madawati hayo wananchi, wadau na taasisi mbalimbali wanapaswa kushirikishwa ili watoto wote wanaoripoti shuleni wapate sehemu ya kukaa.
‘Tunahitaji michango ya hali na mali katika kipindi hiki, naomba taasisi zote zilizopo hapa manispaa zikiwemo asasi za kiraia, vyama vya siasa na watu binafsi washirikishwe ili kufanikisha jambo hilo,’ amesema.
Amebainisha kuwa ataunda Kamati itakayofuatilia michango hiyo hivyo akawataka wajumbe kutoa ushirikiano wa kutosha ili kufanikisha zoezi hilo kwa wakati.
Akichangia hoja hiyo Mjumbe wa Kamati hiyo kutoka Chama cha Wananchi (CUF), Rehema Kabata ameafiki wazo hilo na kuongeza kuwa limekuja kwa muda muafaka kwa kuwa watoto walioandikishwa kuanza shule ni wengi.
Ameomba zoezi hilo lifanyike kwa haraka zaidi ili watoto wote waweze kusomea sehemu nzuri na salama kwa mstakabali wa taifa la kesho.
‘Tunaunga mkono kwa asilimia 100 wazo hili, ila tunashauri liwe endelevu kwani kila mwaka watoto wanajiunga shule za msingi na sekondari na idadi yao inaongezeka kila mwaka kutokana na hamasa kubwa ya serikali, hivyo ni muhimu sana wadau kuchangia’, alisema Rehema.
Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya manispaa hiyo Elias Kayandabila amewataarifu Wajumbe wa Kikao hicho kuwa tayari wametenga fedha za mapato ya ndani kwa ajili ya ununuzi wa madawati 420 ya kuanzia.
Amebainisha kuwa wamelipa kipaumbele kikubwa suala hilo na juhudi za kupata madawati zaidi zinaendelea kufanyika, hivyo akaomba wananchi na wadau mbalimbali kuwaunga mkono ili kuimaliza changamoto hiyo.
Comments
Post a Comment