KATIBU MKUU AMWAGA PONGEZI KWA UWT TABORA
Na Allan Kitwe, DmNewsonline
Tabora
JUMUIYA ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Mkoani Tabora imepongezwa kwa kudumisha umoja na mshikamano miongoni mwao katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani.
Pongezi hizo zimetolewa jana na Katibu Mkuu wa UWT Taifa Suzane Kunambi alipokuwa akiongea na mamia ya Viongozi na wanachama wa Jumuiya hiyo kutoka Wilaya zote 7 za Mkoa huo na vikundi vya wanawake wajasiriamali.
Ameeleza kuwa umoja na mshikamano unaoendelea kuoneshwa na akinamama wa UWT Mkoani hapa na wanaCCM wote ni ishara tosha kuwa wagombea wote wa CCM watapata ushindi wa kishindo.
‘Wanawake wa Tabora hongereni, kazi yenu ni njema sana, naamini Oktoba 29 mwaka huu, mtajitokeza kwa wingi zaidi na kumpigia kura za kishindo mgombea Urais kupitia CCM, wabunge na madiwani, CCM Oyeee’, amesema.
Kunambi amesisitiza kuwa ni wajibu wa wana UWT kushiriki kikamilifu katika kampeni zinazoendelea sasa hapa nchini na kuhakikisha wanakuwa mstari wa mbele kumsemea Dk Samia Suluhu Hassan na kujitokeza kwa wingi kupiga kura.
Amebainisha kuwa wana UWT, wanaCCM na jamii kwa ujumla wana kila sababu ya kumuunga mkono Dkt Samia Suluhu Hassan na kumpigia kura za kutosha kwa kuwa amefanya mambo makubwa katika kipindi kifupi tu cha miaka 4.
‘Hamasa ya akinamama hapa Tabora ni kubwa mno, naomba tukiheshimishe chama chetu Oktoba 29 mwaka huu, kwa kuwapigia kura za kutosha wagombea wote wa CCM ili wapate ushindi wa kishindo’, ameeleza.
Katibu Mkuu amedokeza kuwa Rais Dk Samia Suluhu Hassan ameonesha uwezo mkubwa katika utumishi wake kwa Watanzania katika kipindi cha miaka 4 tu hivyo akipewa miaka mitano tena nchi itapiga hatua kubwa zaidi kimaendeleo.
Comments
Post a Comment