HAMOUD JUMAA:DKT SAMIA AMEILETEA NCHI MAENDELEO .
Mgombea ubunge Jimbo la Kibaha Vijijini Hamoud Jumaa akiwa katika Kata ya Kwala kwa ajili ya kufanya kampeni za kuomba ridhaa Wananchi wamchague Oktoba 29 mwaka huu
Na Gustaphu Haule, DmNewsonline
PWANI
MGOMBEA ubunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini Hamoud Jumaa ( Mzee Sambusa ) amemmwagia sifa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kutokana na ushujaa wake wa kuiletea nchi maendeleo.
Jumaa amesema CCM haina mashaka wala wasiwasi na Dkt .Samia kwakuwa inauhakika na uwezo wake na hata utendaji wake kwani wamemuona katika kipindi chake cha miaka minne alichokaa madarakani.
Jumaa amesema hayo Oktoba 15 ,2025 wakati akizungumza na Wananchi wa Kata ya Kwala ikiwa ni sehemu ya muendelezo wa mikutano yake ya kampeni kwa ajili ya kuomba kura ili ifikapo Oktoba 29 waweze kumchagua kuwa mbunge,kumchagua Rais Samia pamoja na diwani wa Kata hiyo Mansour Kisebengo.
Amesema Dkt.Samia wakati anaingia madarakani wengi walisema hatoweza lakini ameweza kuongoza nchi vizuri na amefanya mambo makubwa ambayo hayakuwai kutokea tangu nchi ipate uhuru .
Amesema kutokana na uwezo wake CCM iliona anafaa kuendelea na ikampitisha katika mchakato wa ndani na sasa ametoka nje kwa ajili ya kumuombea kura ili aweze kushinda kwa kishindo.
Jumaa amesema Dkt.Samia wakati anaingia madarakani alikutana na kipindi kigumu hasa katika kukabiliana na ugonjwa wa Corona ( COVID - 19)lakini mama alisimama vizuri na kuweza kuivusha nchi.
Amesema Rais Dkt. Samia ameweza kununua magari ya wagonjwa 572 jambo ambalo toka uhuru haijawai kutokea na pia amepambana na Bandari ya Dar es Salaam kwa kufanya maamuzi magumu ya kuitoa kampuni ya zamani na kuweka kampuni mpya ya DP WORLD.
Jumaa amesema tangu ilipoingia kampuni mpya ya DP WORLD kumekuwa na mafanikio makubwa kwani ufanisi umeongezeka kutoka kupakua mizigo tani 18000 hadi kufikia tani 32000.
Amesema ongezeko la upakuaji wa tani za mizigo maana yake kumepelekea kuwepo na ongezeko la ajira kwa Watanzania pamoja na ongezeko la mapato kutoka trilioni 18 alizozikuta hadi kufikia trillion 32 katika uongozi wake.
Jumaa amesema mapato hayo yamesaidia kuleta maendeleo kwa kujenga miundombinu mbalimbali ikiwemo ujenzi wa Shule,Zahanati na barabara katika kila eneo nchi Tanzania
Kuhusu Jimbo la Kibaha Vijijini Jumaa amesema Kibaha Vijijini ni sehemu mojawapo iliyonufaika na uongozi wa Dkt.Samia kwani imepata vituo vitatu vya afya ikiwemo Kwala ,Magindu ambapo kituo cha Kwala kilipata Sh. 544 kutoka kwa Dkt.Samia huku akitoa Sh.bilioni 3:534 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya Wilaya,
Jumaa ,amesema pia Kibaha Vijijini imepata Shule nane za Sekondari na Shule mpya tatu za msingi ikiwemo Msua,Mwembengozi na Mkombozi.
Jumaa amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo vitajengwa vituo vingine vitatu vya afya katika Kata ya Boko ,Soga na Ruvu pamoja na kujenga uzio katika hospitali ya Wilaya
Pia amesema yapo mambo makubwa yatafanyika ikiwemo kujenga stendi ya Mlandizi ambapo tayari Sh.milioni 600 zimepatikana,kujenga barabara ya lami katika Mji wa Mlandizi yenye urefu wa Kilomita Moja na kujenga soko la Kisasa la Sh .bilioni 7. 

Comments
Post a Comment