MGOMBEA URAIS WA ADA-TADEA AAHIDI TANZANIA KUMILIKI SATELLITE YAKE ENDAPO ATAPATA RIDHAA YA KUWA RAIS
Na Mwandishi wetu,DmNewsOnline
DAR ES SALAAM
MGOMBEA Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha African Democratic Alliance (ADA -TADEA), Georges Bussungu amesema kwamba endapo atapata ridhaa ya kuwa Rais atahakikisha Tanzania inamiliki Satellite yake
Akizungumza katika uzinduzi wa kampeni za Chama hicho Leo Septemba 14,2025 katika Viwanja vya Zakhem Mbagala Jijini Dar es Salaam amesema kwamba vipaumbele vya Ilani ya chama itahakikisha inajenga kituo maalum cha teknolojia nchini kitakachoitwa Bongo Selcom City ambacho kitasimamia masuala yote yahusuyo Teknolojia kwani teknolojia ndio inayotumika sana duniani
Aidha amesema wataleta mapinduzi ya kifikra kwa watanzania kwa kuanzisha elimu ya kujitegemea kuanzia elimu ya chekechea hadi chuo kikuu kwa kujifunza elimu ya nadhalia ili kuwapatia elimu iliyobora na yakujitegemea na namna yakujiari wenyewe
Pia amesema atahakikisha kuweka mazingira Bora kwa wakulima ili kilimo kiwe Bora na chenye tija kwa wananchi kwa kuwapatia kila Kitongoji paratila Moja na Kila kijiji kuwa na trekta kwa ajili yakuwasaidia wakulima wadogo.
Aliendelea kwamba atahakikisha serikali yake itaanzisha mashamba makubwa ya mazao mbalimbali nchini ambayo yatazalisha na kuwaletea wananchi kipato na kuingiza mapato Serikalini ilikukuza uchumi wa nchi
Kwa upande wake Mwenyekiti wa ADA-TADEA ,Juma Ally Khatibu ameishukuru Tume Huru ya Uchaguzi(INEC) kwa kutoa magari kwa wagombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka vyama mbalimbali vya siasa
Amesema magari hayo yanawawezesha wagombea wa Urais kuwafikia wananchi kwa urahisi ili kunadi sera za vyama vyao na kuomba ridhaa.
Pia ameeleza kwamba endapo watapata ridhaa yakuongoza nchi katika uchaguzi mkuu ujao,Serikali ya chama itahakikisha kuwa kila mama anayejifungua nchini atapatiwa maziwa Bure kwa ajili ya watoto wake.
"Wapo wanawake ambao wanachangamoto zinaziwakabili wakati wakujifungua ambao wanashindwa kumudu huduma za uzazi hali inayopelekea wengine kutupa watoto", amesema Mwenyekiti Khatibu
Aliongeza kwamba Serikali yake itajitahidi kuboresha huduma za afya na kuangalia maslahi ya wazee waliostaafu na wanaotegemea msaada,hivyo watahakikisha kila mzee anapatiwa kiasi cha pesa ili kuweza kumudu maisha yake.
Hata hivyo Mwenyekiti Juma Ally Khatibu amezindua rasmi Ilani ya Uchaguzi ya Chama na kuwapatia wagombea wa Urais ili waweze kwenda kuinadi.
Uzinduzi wa kampeni hizo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama,wanachama pamoja na wagombea Ubunge na Udiwani wa Chama hicho 

Comments
Post a Comment