MGOMBEA UDIWANI CCM AAHIDI NEEMA KWA WANANCHI
KALIUA
MGOMBEA udiwani wa Kata ya Ukumbisiganga, Wilayani Kaliua Mkoani Tabora Andrea Makoba kupitia CCM amewataka wakazi wa Kata hiyo kuchagua wagombea wa chama hicho kwa kuwa kina ilani iliyojaa neema ya maendeleo kwa wananchi.
Akihutubia umati wa wanaCCM na wakazi wa Kitongoji cha Usinga namba 78 katika Kijiji cha Usinga (maarufu kama km 90) amesema kuwa wakazi wa Kijiji hicho wana kila sababu ya kuishukuru serikali ya CCM kwa mambo makubwa iliyowafanyia.
Amebainisha kuwa katika kipindi cha miaka 4 tu tangu Rais wa Awamu ya Sita, Dk Samia Suluhu Hassan aingie madarakani, Kata hiyo imeneemeka kwa kupata Kituo cha Afya ambacho kipo katika hatua mwisho za ukamilishaji.
Ameongeza kuwa Kituo hicho ni mkombozi kwa akinamama wajawazito na jamii kwa ujumla kwa kitamaliza kero wanayopata sasa ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za matibabu katika hospitali ya Wilaya Mjini Kaliua.
Mambo mengine yaliyofanywa na Rais Samia Kijijini hapo ni kutekelezwa kwa mradi wa maji safi na salama ya kisima ambao umewezesha wakazi wa Kijiji hicho kupata huduma ya maji safi na salama ya kunywa tofauti na miaka ya nyuma.
Aidha vyumba vya madarasa katika shule ya msingi Usinga na Ukumbi Kakoko vimeboreshwa kwa kiasi kikubwa na kufanya shule hizo kuwa na mazingira bora ya kusomea watoto.
‘Ilani mpya ya uchaguzi ya CCM ya 2025-2030 ina mambo mazuri sana, mpeni mitano tena Dkt Samia Suluhu Hassan ili ashushe neema ya maendeleo hapa Ukumbisiganga, Josephat Mtama awe mbunge na Andrea Makoba diwani’, amesema.
Katibu Kata wa CCM, Mfaume Abdallah amedokeza kuwa wakazi wa Kata hiyo wanaishukuru sana serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia kwa kuwaruhusu waendelee kuishi eneo hilo na kuomba Kijiji hicho kitambuliwe rasmi.
Amesisitiza kuwa wakazi wa eneo hilo wakiwemo wachache wa vyama vya upinzania, wote wamekunwa na utendaji wa Rais Samia na wameahidi kumpa kura za kishindo ili aendelee kuwafanyia mambo makubwa zaidi kwa mwaka 2025-2030.
Wakiongea kwa nyakati tofauti katika mkutano huo Dafroza Damas na Paulina Damas wamepongeza maboresho makubwa ya huduma za kijamii yaliyofanyika katika Kijiji hicho na kubainisha kuwa miaka 5 ijayo Mama atafanya makubwa zaidi. 

Comments
Post a Comment