KONGAMANO LA KITAIFA LA WADAU WA UCHUMI WA BULUU LAFANYIKA JIJINI DAR ES SALAAM
Na Mwandishi wetu,DmNewsonline
DAR ES SALAAM
KONGAMANO la Kitaifa la Wadau wa Uchumi wa Buluu limeanza leo Septemba 10 ,2025 Jijini Dar es Salaam nw linatarajiwa kufanyika kwa siku mbili mfululizo hadi Septemba 11, 2025.
Mgeni rasmi katika Kongamano Hilo ni Naibu Katibu Mkuu (Muungano) kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Abdallah Mitawi amesema kwamba Serikali imedhamiria kutumia ipasavyo rasilimali za bahari na maji ya ndani kwa maendeleo endelevu ya Taifa.
“Uchumi wa buluu ni injini mpya ya maendeleo ya Tanzania. Ukitumiwa kwa ufanisi unaweza kuongeza ajira, kukuza biashara na kuimarisha ustawi wa wananchi,” amesema Mitawi.
Naye mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Mkurugenzi wa Miundombinu ya Uchukuzi, Mhandisi Shomari Shomari, amesema maboresho ya miundombinu ya bandari, reli na vyombo vya usafiri majini ni nguzo muhimu za kukuza uchumi wa buluu na kuongeza ushindani wa biashara kitaifa na kimataifa.
Aidha,ametoa wito kwa wadau wote kushirikiana ili kuhakikisha miradi ya usafirishaji inaleta manufaa kwa Taifa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI), Prof. Tumaini Gurumo, amesema chuo hicho kina jukumu la kutoa elimu, kufanya tafiti na kuzalisha wataalamu wanaohitajika katika sekta za bahari, usafirishaji na uhifadhi wa mazingira ya pwani.
“DMI ni nguzo muhimu ya maendeleo ya uchumi wa buluu kwa kuwaandaa vijana kushiriki kikamilifu kwenye sekta hii,” amesema Prof. Gurumo.
Kongamano hili limeandaliwa kwa ushirikiano wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Wizara ya Uchukuzi kupitia DMI, na Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi – Zanzibar, likiwa na lengo la kuunganisha wadau na kuweka mikakati ya kitaifa ya kuendeleza uchumi wa buluu kwa njia endelevu 

Comments
Post a Comment