“Doyo. Sitavumilia Mfumo wa Stakabadhi Ghalani, Madini ya Tanzanite Yawanufaishe Wananchi wa Manyara”
Na Mwandishi wetu,DmNewsOnline
BABATI ,MANYARA
MGOMBEA Urais kupitia Chama cha NLD, Mhe. Doyo Hassan Doyo, leo tarehe 15 Septemba 2025, ameendelea na ziara yake ya kampeni mkoani Manyara katika vijiji vya Bonga, Hala, Nakwa, Sigino na Posta (Singu), na kukamilisha mkutano wake wa kampeni Babati mjini.
Akihutubia wananchi mjini Babati, Mhe. Doyo alilalamikia mfumo wa stakabadhi ghalani unaotumika katika zao la mbaazi, akisema kuwa mfumo huo hauwanufaishi wakulima wadogo wa Manyara na Tanzania kwa ujumla. Alifafanua kuwa wakulima hulima kwa gharama zao, hununua pembejeo kwa fedha zao na hulinda mashamba yao kwa gharama kubwa, lakini wanapofika sokoni hulazimishwa kuuza mazao yao kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani kwa bei ya chini.
“Wakati mnapouza kilo kati ya shilingi 700 hadi 1,700 tu, wapo wanunuzi binafsi waliokuwa tayari kulipa hadi shilingi 3,500 kwa kilo. Hii ni dhuluma kwa mkulima. Nikipewa ridhaa ya kuwa Rais, nitahakikisha mkulima anauza mazao yake kwa bei ya soko huru na si kwa kulazimishwa na mfumo wa stakabadhi ghalani, unaowanufaisha watu wachache,” amesema Doyo.
Akiendelea kueleza, Doyo alisema bei ya mbaazi imeshuka kutoka shilingi 3,000 kwa kilo hadi shilingi 700, hali iliyosababisha gunia la mbaazi kushuka kutoka wastani wa shilingi 300,000 hadi shilingi 70,000 pekee. Alisema hali hiyo ni mzigo mkubwa kwa wakulima wa Manyara na mikoa mingine inayozalisha zao hilo Tanzania.
Aidha, kuhusu rasilimali za madini, Doyo aligusia madini ya Tanzanite yanayopatikana Simanjiro, Manyara pekee duniani. Alisema wananchi wa Manyara hawajanufaika moja kwa moja na rasilimali hiyo licha ya kuwa Madina hayo yanapatikana Manyara kipekee, na kutoa mfano wa baadhi ya nchi za Kiarabu ambapo wananchi hunufaika moja kwa moja na mafuta yanayopatikana nchini mwao kwa kuondolewa baadhi ya kodi.
“Iwapo angalau asilimia 40 ya mapato ya madini yangerudi moja kwa moja katika halmashauri za mikoa inayopatikana Madina hayo, wananchi wangepata huduma bora za kijamii. Nikichaguliwa kuwa Rais, nitahakikisha wananchi wa Manyara wananufaika na Tanzanite yenu,” amesema Doyo.
Mhe. Doyo aliwataka wananchi wa Manyara kufanya maamuzi sahihi katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29 kwa kumpa kura yeye kama rais, na mgombea ubunge wa Babati Mjini kupitia Chama cha NLD Ndugu Paschal Bruno Ngomuo, na mgombea udiwani Andrea Abraham Kiula. Alisisitiza kuwa Manyara itakuwa kituo cha utalii baada ya Arusha, na vijana wa Babati watanufaika na fursa za kiuchumi kupitia utalii.
Kwa upande wake, mgombea ubunge wa Babati Mjini kupitia NLD, Ndugu Paschal Bruno Ngomuo, alisema wananchi wanapewa nafasi ya kuchagua kiongozi sahihi atakayepigania maslahi yao. Aliahidi kushirikiana na mamlaka husika kuhakikisha Geti la Mamire linatambulika kama lango la utalii, tofauti na ilivyo sasa ambapo wageni wengi hutumia Minjingu na Kibao cha Tembo karibu na Magugu.
“Wananchi wa Babati, kupanga ni kuchagua. Mkinichagua mimi nitakuwa sauti yenu, nitalinda maslahi yenu na kuhakikisha mnafaidika na bei nzuri za mazao yenu. Mkiendelea kuchagua viongozi wa sasa, mtabaki na bei zisizo na faida kwenu,” amesema Ngomuo.
Msafara wa mgombea urais huyo wa NLD unaelekea Arusha kuendelea na kampeni zake, ukiongozwa na kaulimbiu ya “Uzalendo, Haki na Maendeleo kama dira ya Ilani ya Uchaguzi.” 

Comments
Post a Comment