BILIONI 220 ZABORESHA HUDUMA ZA JAMII MANISPAA TABORA

    Na Allan Kitwe,DmNewsonline 

                   TABORA 

SERIKAli ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dk Samia Suluhu Hassan  imepekeleka zaidi ya shilingi bilioni 220 katika Halmashauri ya Manispaa Tabora katika kipindi cha miaka 4 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.

Fedha hizo zimeleta mageuzi makubwa katika sekta ya elimu na afya kwa kuboreshwa miundombinu ya shule zote za msingi na sekondari na kutatua kero ya upatikanaji huduma bora za afya katika manispaa hiyo.

Hayo yameelezwa na Mgombea Ubunge wa Jimbo la Tabora Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Hawa Mwaifunga kwenye mkutano wa uzinduzi wa kampeni za CCM uliofanyika jana katika uwanja wa Taasisi katika manispaa hiyo.

Amesema kuwa wakazi wa manispaa hiyo na Mkoa mzima wa Tabora wana kila sababu ya kumpigia kura za kishindo mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM kwa kuwa amewafanyia mambo makubwa.

‘Katika kipindi cha miaka nne na nusu tu aliyokaa madarakani, Rais Dk Samia Suluhu Hassan ameleta takribani shilingi bilioni 228 za miradi katika Jimbo hili ili kuharakisha maendeleo ya wananchi, hili ni jambo kubwa sana’, ameeleza.

‘Wakazi wa manispaa Tabora nawaombeni sana ifikapo Oktoba 29 mwaka huu twende tukampigie kura za kishindo mgombea Urais kupitia CCM, Dk Samia, mgombea ubunge Mwaifunga na wagombea udiwani wa CCM wote’, amesema.

Mwaifunga amefafanua mambo yaliyofanyika katika Jimbo hilo kuwa ni ujenzi wa shule mpya za sekondari na msingi na kuboreshwa vyumba vya madarasa, ofisi za walimu na matundu vyoo vilivyokuwa vimechakaa katika shule zote.

Ametaja baadhi ya kata ambazo zimenufaika na miradi hiyo na jamii kunufaika kwa kiasi kikubwa sana kuwa ni Ifucha, Kakola, Isevya, Ndevelwa, Mbugani, Mapambano, Kalunde, Kabila, Itetemia, Kitete na nyinginezo.

Kwa upande wa huduma za afya amesema kuwa Vituo vya afya vimejengwa katika kata za Kakola, Kabila, Uyui na Ikomwa na kuboreshwa miundombinu ya utoaji huduma za afya katika Vituo mbalimbali vya afya na zahanati.

Aidha ameeleza kuwa katika kipindi cha miaka minne serikali ya awamu ya sita imeongeza ikama ya watumishi katika sekta ya elimu na afya hivyo kupunguza kwa kiasi kikubwa uhaba wa watumishi katika manispaa hiyo.   

Comments

Popular posts from this blog

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE TAMISEMI YAKOSHWA NA UBORA WA MIRADI YA MAENDELEO KIBAHA TC

MAMBO 10 MAZITO YANAYOIANGAMIZA NA KUIZAMISHA CHADEMA 2024/2025