AMICI DELLA TANZANIA WATOA MSAADA WA KOMPUTA SHULE YA MSINGI KIPALAPALA

  Na Allan Kitwe, DmNewsonline

                 TABORA 

TAASISI ya Amici Della Tanzania (Marafiki wa Tanzania) ya nchini Italia imetoa msaada wa komputa mpakato (laptops) 10 zenye thamani ya sh milioni 6 katika shule ya msingi Kipalapala iliyopo katika kata ya Itetemia Mjini Tabora.

Akizungumza na walimu na wanafunzi wa shule hiyo baada ya kukabidhi vifaa hivyo jana, Mwenyekiti wa Taasisi hiyo kutoka nchini Italia Hapiphana Lubangula amesema kuwa wametoa msaada huo ili kuboresha utoaji elimu katika shule hiyo.

Amebainisha kuwa vifaa hivyo vitasaidia watoto wa shule hiyo kusoma kwa bidii na watakapomaliza shule ya msingi na kuendelea sekondari wawe na uwezo mkubwa wa kutumia komputa (tarakirishi).   

Mbali na vifaa hivyo Lubangula amesema kuwa pia wanagharamia upakaji rangi kwenye vyumba vya madarasa vyote, ofisi za walimu na wataleta umeme katika shule hiyo ili kuwezesha watoto kusoma katika mazingira bora zaidi.

Amesisitiza kuwa maendeleo ya mtoto ni maendeleo ya nchi nzima hivyo mtoto akisomea mahali pazuri atasoma kwa bidii na kuwa na ufaulu mzuri katika mitihani yake ya mwisho na hatimaye aweze kutimiza ndoto zake.

‘Mimi nimezaliwa hapa Kipalapala, hivyo nimekuja kutoa fadhila katika shule yetu, tunataka shule hii ipendeze na iwe na maendeleo makubwa na watoto wasome kwa bidii ili wafike mbali na kusaidia wazazi wao’, amesema.  

Mwenyekiti wa Kamati ya Shule hiyo Mtemi Msagata Fundikira (Mtemi wa Unyanyembe) ameishukuru Familia ya Lubangula kwa msaada waliotoa kwa shule hiyo na kuomba wadau wengine kuiga mfano huo.

Ameeleza kuwa msaada waliotoa kwa shule hiyo ni chachu kubwa kwa maendeleo ya shule hiyo kwani miundombinu yake hususani vyumba vya madarasa, ofisi na sakafu vimechakaa sana na haina umeme pia.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Masumbuko Muyonga amemshukuru dada Hapiphania Lubangula na wenzake kwa moyo wao wa upendo kwa shule hiyo, aliahidi kuwa watatumia vizuri komputa hizo na kutunza vizuri miundombinu.

Aidha ameeleza kufurahishwa na msaada wa Taasisi hiyo wa kuwaletea umeme kwani utakapofika utawarahisishia utekelezaji majukumu yao ikiwemo kutumia komputa walizopewa kuchapa taarifa za wanafunzi na kuandaa mitihani.   

Comments

Popular posts from this blog

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE TAMISEMI YAKOSHWA NA UBORA WA MIRADI YA MAENDELEO KIBAHA TC

MAMBO 10 MAZITO YANAYOIANGAMIZA NA KUIZAMISHA CHADEMA 2024/2025