NFRA YATOA ELIMU JUU YA UHIFAFDHI WA CHAKULA
Na Richard Mrusha,DmNewsOnline
Dar es salaama
Afisa Masoko wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Bi Eva Michael, amewaeleza wananchi kuhusu majukumu na huduma mbalimbali zinazotolewa na wakala huo, wakati wakishiriki kwenye Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara yanayofanyika jijini Dar es Salaam.
Katika maonesho hayo, NFRA imejipanga kutoa elimu kwa wananchi, wakulima pamoja na wafanyabiashara juu ya masuala ya uhifadhi salama wa chakula, sambamba na kueleza nafasi ya kila mmoja katika kuhakikisha Taifa linakuwa na akiba ya kutosha ya chakula kwa ajili ya usalama wa chakula na matumizi ya dharura.
Bi Eva Michael amesema kuwa moja ya majukumu makuu ya NFRA ni kununua, kuhifadhi na kuuza nafaka. Kwa sasa, taasisi hiyo iko katika maandalizi ya awali ya msimu mpya wa ununuzi wa nafaka kutoka kwa wakulima nchini. Lengo ni kuhakikisha kuwa wakulima wanapata soko la uhakika huku Taifa likijihakikishia akiba ya chakula ya kutosha.
Kwa mujibu wa Bi Eva, kwa sasa NFRA ina aina mbalimbali za nafaka zilizopo kwenye maghala yao zikiwemo mahindi,mpunga,mtama mweupe,Mbaazi na dengu
Aidha, NFRA inaendelea na mauzo ya nafaka hizo kwa wadau mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara wa ndani na wa nje ya nchi. Bi Eva amethibitisha kuwa kiwango kikubwa cha nafaka kimehifadhiwa katika mazingira salama, na kwamba taasisi hiyo iko tayari kushirikiana na wadau wote wanaotaka kufanya biashara ya kununua au kuuza nafaka kupitia NFRA.
“Niwakaribishe wadau wote—wafanyabiashara, wakulima na wananchi wa kawaida—kutembelea banda letu hapa maonesho ili kupata elimu ya uhifadhi, lakini pia kujua fursa mbalimbali zinazotolewa na NFRA,” amesema Bi Eva.
Comments
Post a Comment