MA-DC TATUENI KERO ZA WANANCHI...

    Na Allan Kitwe,DmNewsonline

              TABORA

WAKUU wapya wa Wilaya walioteuliwa hivi karibuni na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika Mkoa wa Tabora wametakiwa kuwa karibu zaidi na wananchi, kusikiliza kero zao na kuzitafutia ufumbuzi ili kumaliza kero zinazowakabili.

Wito huo umetolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Paul Chacha alipokuwa akimwapisha Mkuu wa Wilaya ya Sikonge, Thomas Myinga na wa Tabora Mjini Upendo Wella katika ukumbi wa Mtemi Isike Mwanakiyungi mjini hapa.

Amesema kuwa kila mteule wa Rais aliyeletwa katika Mkoa huo amekuja kuhudumia wananchi, si vinginevyo, hivyo anapaswa kuwa karibu zaidi na wananchi, kusikiliza kero zao na kuzitafutia ufumbuzi.

Ili kufanikisha utekelezaji majukumu yao kwa tija amewataka kushirikiana kwa karibu zaidi na viongozi wa kiroho, watumishi walio chini yao, taasisi za umma na zisizo za umma, mashirika na wadau wote wa maendeleo.

RC Chacha amesisitiza kuwa Mheshimiwa Rais ana imani kubwa na wote aliowateua katika nafasi mbalimbali ikiwemo za Ukuu wa Mikoa, Ukuu wa Wilaya, Ukurugenzi, Ukatibu Tawala wa Mkoa na Wilaya, hivyo wasimwangushe.

‘Miradi mingi ya maendeleo tena ya mabilioni ya fedha inaendelea kutekelezwa katika wilaya zote za Mkoa huo, ni jukumu lenu kuhakikisha inatekelezwa kikamilifu na kwa weledi mkubwa wananchi wanufaike nayo’, amesema.

Awali Katibu Tawala wa Mkoa huo Dkt John Mboya aliwaeleza kuwa Rais Dkt Samia ameleta zaidi ya shilingi bilioni 270 katika Mkoa huo kwa ajili ya miradi ya maendeleo, hivyo akawataka kuisimamia ipasavyo na ikamilike kwa wakati.

Aidha amewataka kusimamia maadili ya jamii katika maeneo yao, kuhakikisha fedha za lishe zinazoletwa zinatumika ipasavyo katika Wilaya zao ili kutokomeza udumavu wa watoto na kuimarisha upatikanaji lishe bora.

Pia amesisitiza Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa halmashauri zote 8 za Mkoa huo kuwa na mikakati endelevu ya utunzaji mazingira katika maeneo yao na kuchukua hatua madhubuti za kukomesha vitendo vya uharibifu wa miti.

Akiongea katika hafla hiyo Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora Said Nkumba amewataka kuwa wawakilishi wazuri wa Mheshimiwa Rais katika wilaya zao kwa kuwatumikia wananchi ipasavyo na kuzingatia maadili ya kazi zao.  


Comments

Popular posts from this blog

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE TAMISEMI YAKOSHWA NA UBORA WA MIRADI YA MAENDELEO KIBAHA TC

MAMBO 10 MAZITO YANAYOIANGAMIZA NA KUIZAMISHA CHADEMA 2024/2025