RC KUNENGE ARIDHISHWA NA KASI YA UKUSANYAJI WA MAPATO HALMASHAURI YA KIBAHA TC
KIBAHA
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Alhaji Abubakari Kunenge amempongeza kwa dhati Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Kibaha mjini Dkt.Rogers Shemwelekwa kwa kuweza kuweka mikakati madhubuti katika kubuni vyanzo vipya vya ukusanyaji wa mapato ya ndani ambayo yameweza kuleta mabadiliko chanya katika utekelezaji wa miradi mbali mbali ya kimaendeleo.
Kunenge ameyasema hayo wakati wa kikao maalumu cha baraza la madiwani katika Halmashauri ya Kibaha mji kwa ajili ya kuweza kujadili taarifa ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali (CAG) kwa kipindi cha kuanzia mwaka wa 2023 hadi 2024 ambacho kimeweza kuhudhuliwa na viongozi mbali mbali wa serikali, wakuu wa idara, wataalamu pamoja na viongozi mbali mbali wa chama.
Amesema kwamba Halmashauri ya Kibaha mji imeweza kupiga hatua kubwa hadi kuweza kupandishwa hadhi ya kuwa Manispaa kutokana na juhudi na ushirikiano ambao unafanya na viongozi mbali mbali wakiwemo wakuu wa idara, baraza la madiwani,mkuu wa Wilaya pamoja na Mkurugenzi mtendaji kwa kuweza kushirikiana na viongozi wenzake katika suala zima la kuleta maendeleo katika nyaja mbali mbali.
"Nampongeza sana Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Kibaha mjini Dkt. Rogers Shemwelekwa pamoja na timu yake nzima wakiwemo wakuu wa idara, wataaalamu pamoja na baraza la madiwani ambao kwa kweli mimi siwezi kuoana sababu ya kutowapongeza kwa dhati kabisa akiwemo Mbunge pamoja na Mkuu wa Wilaya ambao wameunganisha umoja na ushirikiano katika suala zima la maendeleo bila kusahau juhudi za kupandisha hadhi kuwa Manispaa,"amebainisha Kunenge.
Aidha Kunenge amewataka viongozi wa Halmashauri ya Kibaha mji kuachana na tabia ya kuwa na mivulugano na vurugu ambazo hazina tija na badala yake wahakikishe wahakikishe wanaungana kwa pamoja katika kusikiliza na kushughulikia kero na changamoto mbali mbali zinazowakabili wananchi.
Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Kibaha mjini Dkt. Rogers Shemwelekwa amempongeza Rais wa awamu ya sita Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kutenga fedha nyingi ambazo zimeweza kwenda kutekeleza miradi mbali mbali ya maendeleo ikiwemo katika sekta ya afya, maji, elimu, miundombinu ya barabara pamoja na huduma nyingine za msingi.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kibaha mjini Mussa Ndomba amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na baraza la madiwani kwa kuweza kushirikiana bega kwa bega katika kipindi chote cha miaka mitano hali ambayo imeweza kuleta mabadiliko makubwa katika suala zima la kuweza kuongeza kasi kubwa ya maendeleo kwa wananchi. 

Comments
Post a Comment